Sunday, 23 August 2015

Magazeti Hizi ndio stori kwenye kurasa za mbele na za nyuma Magazeti ya Tanzania August 23 2015..

Leave a Comment

SUND
MWANANCHI
Miezi kadhaa baada ya treni ya kubeba abiria jijini Dar es salaam kusitisha safari zake kutokana na ubovu, imeelezwa kuwa hali hiyo inatokana na uchakavu wa injini.
Mkuu wa masoko wa kampuni ya Reli Tanzania Charles Ndenge alisema treni hiyo imekua ikiharibika mara kwa mara kutokana na injini zake kutumika kwa muda mrefu huku ikifanya kazi tofauti na ilivyoundwa.
“Treni hii ilitengenezwa kwa safari za mbali, hata hivyo imefanya kazi kwa muda mrefu na injini zake zimechoka ndio maana zinafanyiwa marekebisho, niwahakikishie watumiaji huduma ya usafiri itarejea kama kawaida” Ndenge.
Alifafanua mpaka sasa matengenezo yamefikia hatua nzuri na wiki mbili zijazo huduma hiyo itaanza kufanya kazi tena.
HABARILEO
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga imewatia hatiani watu sita na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kuua kwa kukusudia. Waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni Oden Msongela , Philibert Majaliwa , Edwin Simba , Sabas Alfred,Wenseslaus Kakwale na Maiko Simfukwe. Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mwakipombe Sango.
Watu hao wamepatikana na hatia ya kumuua kwa kukusudia kwa kumpasua fuvu mkazi wa kijiji cha Lusaka, wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa, Maiko Hussein (56).
Baada ya Jaji Sambo kusikiliza ushahidi aliwahukumu washitakiwa sita kifo huku wengine wawili wakiachiwa huru.
Walioachiwa huru ni Gilbert Mwanandenje  na Meresi Namazali . Waliachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kutoa ushahidi usiotia shaka mahakamani hapo.
“Mahakama hii imewatia hatiani washtakiwa hawa sita kwa kosa la kuua kwa kukusudia baada ya kujiridhisha na aina ya silaha zilizotumika zikiwemo nondo, mashoka , panga na marungu , pia nguvu kubwa iliyotumika kushambulia na madhara yaliyosababishwa na kipigo,” alisema.
Jaji Sambo alisema mashahidi wote sita walioitwa mahakamani na upande wa mashtaka wametoa ushahidi, ambao haukuwa na mashaka yoyote, hivyo kuwatia hatiani watu hao sita kwa kosa la mauaji.
“Ushahidi uliotolewa wa utambuzi wa washtakiwa ulikidhi viwango vinavyohitajika katika mashauri ya jinai… hakika ulikuwa umeenea, hivyo nawahukumu kunyongwa mpaka kufa,” alisema Jaji Sambo wakati akisoma hukumu hiyo.
Upande wa mashitaka uliongozwa na Mwanasheria wa Serikali, Scholastica Lugongo huku washtakiwa hao wakitetewa na wakili wa kujitegemea , Mathias Budodi. Awali kabla ya hukumu hiyo, ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ulieleza kuwa Hussein alitendewa unyama huo Mei 13 , 2012 katika kijiji cha Lusaka, wilaya ya Sumbawanga kati ya saa tatu na saa nne usiku.
Inadaiwa kuwa Hussein usiku huo alikuwa na mkewe Winfrida ambapo washtakiwa hao walibisha mlango na walipofunguliwa waliingia ndani na kumkamata marehemu na kumtoa nje ya nyumba yake na kuanza kumpiga.
Ushahidi huo unaeleza kuwa Hussein alifanikiwa kuwachomoka washtakiwa hao na kuanza kutimua mbio lakini walimfukuza hadi wakamkamata na kuanza kumshambulia kwa silaha za jadi kisha mmoja wao akampiga kwa panga kichwani na kumpasua fuvu lake .
Ilielezwa kuwa baada ya kufanya mauaji hayo washtakiwa hao waliufunika mwili huo kwa nyasi kisha wakauteketeza kwa moto . Watuhumiwa hao pia wanadaiwa kuteketeza nyumba hiyo ya marehemu na nyumba nyingine tano katika kijiji hicho cha Lusaka wakiwatuhumu wenye nyumba hizo kuwa ni wachawi.
HABARILEO
Mkazi wa Gogoni kata ya Dunda wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Ramadhan Mlala anatuhumiwa kumuua mke wake Angelina Pius kwa kumchoma na kisu sehemu mbalimbali za mwili wake kutokana na wivu wa mapenzi, akiwa katika ofisi za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Baada ya tukio hilo mtuhumiwa huyo naye kwa kutumia kisu hicho alijichoma tumboni na kutaka kujiua na kusababisha utumbo wake kutoka nje.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jafar Ibrahim alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 21 mwaka huu majira ya saa tatu asubuhi eneo la Gogoni, kata ya Dunda ambapo chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi.
“Mtuhumiwa alimshambulia mke wake akiwa mlangoni kwenye ofisi za Bakwata alikokwenda kupeleka malalamiko yake ndipo alipomvamia na kumchoma kisu sehemu mbalimbali za mwili wake hadi kufa,” alisema Kamanda Ibrahim.
Kamanda Ibrahim alisema kuwa kabla ya mkasa huo kutokea, wanandoa hao walikuwa na mgogoro wa ndoa wa muda mrefu huku Angelina akidai talaka mara kwa mara baada ya kuona hakuna suluhu zaidi ya kuachana na mumewe huyo.
Kamanda Ibrahim alisema mtuhumiwa huyo kwa sasa anapatiwa matibabu chini ya uangalizi wa jeshi hilo ili akipona ajibu tuhuma zinazomkabili za mauaji ya kukusudia na kuwa kisu alichofanyia mauaji hayo kimepatikana.
HABARILEO
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinatarajiwa kuzindua kampeni zake za urais, ubunge na udiwani nchi nzima katika viwanja vya Jangwani leo, katika mkutano utakaorushwa moja kwa moja na televisheni na redio mbalimbali nchi nzima.
Katika uzinduzi huo, CCM pia inatarajiwa kuweka ilani yake ya uchaguzi hadharani, itakayonadiwa na mgombea urais wake, Dk John Magufuli na wagombea wengine wa ubunge na udiwani nchi nzima.
Moja ya mambo ambayo CCM inatarajiwa kufafanua ni matumaini makubwa ya uwezo wa mgombea wake katika kusimamia utekelezaji wa ilani hiyo, kutokana na historia yake ya utendaji ndani ya Serikali katika nafasi mbalimbali alizokabidhiwa, ikiwemo Waziri wa Ujenzi.
Wageni mbalimbali pia wamealikwa kuhudhuria uzinduzi huo vikiwemo pia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Msemaji wa CCM Mkoa, Juma Simba vile vile wanatarajia wageni kutoka ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam kuhudhuria mkutano huo leo. “Tumetuma mialiko ya mkutano wa kesho (leo) sio tu kwa wana CCM wenzetu bali pia kwa vyama vingine vya siasa ikiwa ni pamoja na kwa vyama vya ‘Ukawa’,” alisema.
Simba alisema mkutano huo utakuwa mkubwa na wa aina yake ambapo viongozi mbalimbali wa chama wanatarajiwa kushiriki na kwamba mkutano huo ratiba yake itaanza asubuhi saa tatu kwa burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali na wananchi kuendelea kuwasili uwanjani.
Sifa za Magufuli Mgombea huyo amekuwa akitajwa kuwa na sifa ya mchapakazi, makini, asiyependa uvivu, ambapo Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alimpachika jina “Tingatinga”.
Rais Kikwete alimpachika Magufuli jina hilo, baada ya kutangazwa kuwashinda makada wengine wawili waliokuwa wakiwania kuteuliwa kuwania urais kupitia chama hicho katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika Dodoma. “Kila mtu anaitwa jembe lakini huyu ni zaidi ya jembe.
Ni tingatinga… Magufuli ni bulldozer. Magufuli havumilii ujinga, ni mtu ambaye anataka kuona kazi zake zinafanyika kama alivyoagiza,” alikaririwa akisema.
Kikwete aliendelea kummwagia sifa Dk Magufuli kuhusu utendaji wake akisema kuwa alipokuwa akifuatilia makandarasi kwenye miradi ya ujenzi, alidiriki kuwatimua pale alipobaini walikuwa wakifanya kazi kinyume na makubaliano.
Baadhi ya watu waliofanya naye kazi wamekaririwa wakisema iwapo atachaguliwa kuwa rais basi wavivu wajitayarishe kukimbia kwani Waziri huyo ni mchapa kazi wa hali ya juu.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mussa Iyombe, aliyefanya kazi na Dk Magufuli kwa zaidi ya miaka 10, alikaririwa akisema kwa kipindi alichofanya kazi na Magufuli ameshuhudia kuwa hataki mchezo katika kazi, hana mzaha na mwenye umakini mkubwa kwa kila anachofanya.
If You Enjoyed This, Take 5 Seconds To Share It

0 comments: